Advertisements

Saturday, October 1, 2016

KUPANDA, KUSHUKA KWA ASHANTI UNITED

UKIKATIZA mitaa ya Ilala, hususani maeneo ya soko la Boma utakutana na shamrashamra za wauza mitumba ambao wanaendelea na shuguli zao za kujipatia riziki na cha kufurahisha ni vigoma vyao na nyimbo wakitangaza bei ‘Mia tanoo... elfu mbili...elfu mojaaa!’.
Lakini wauza mitumba hao wamekuwa chachu ya kuwepo kwa timu ya soka ya Ashanti United ‘Watoto wa Ilala’ kama wanavyoiita wenyewe katika harakati zake zote za kupanda na kushuka kwenye medani ya soka. Unapofika maeneo ya Ilala, makao makuu ya klabu hiyo yanatazamana na jengo la Mwalimu House, ni jengo dogo na chini yake kuna ofisi za DAWASCO au muulize muuza mitumba, yeyote bila shaka atakuonesha ilipo klabu hiyo.
Hata hivyo, klabu hiyo imepita milima na mabonde mpaka ilipo sasa, Katibu mkuu wa Ashanti United, Jimmy China anaelezea milima na mabonde ya Ashanti ambayo ni timu kongwe yenye zaidi ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. “Kiuhalisia ni Ashanti Sports Club ilitokana na timu ya Utete boys ambayo ilikusanya vijana wa Ilala wakina Hamis Kisiwa, Arthar Mwambeta, Juma Mkange, Abdallah Kibadeni hao wote baadae walikuja kuzichezea Simba na Yanga,” anasema China.
Anasema miaka ya 50 jeshi la wanamaji Uingereza walifanya ziara katika nchi ambazo zilikuwa koloni la Muingereza ambako walifika nchini na kucheza mchezo wa kirafiki na Utete Boys iliyoshinda mabao 2-1.

“Hii timu ya Jeshi la Wanamaji la Uingereza ilizunguka nchi nyingi za Afrika nakumbuka ilitokea Ghana ndio ikaja nchini, Ghana ilicheza na Asante Kotoko na Kotoko ilifungwa mabao 2-0. “Mfalme wa Ghana alikuwa kabila la ‘Waashanti’wakati ule akawakabidhi ngao yenye nembo ya Nungunungu ambayo ni nembo ya kabila la Waashanti nchini Ghana. “Walipofika hapa Utete boys wakawanyuka bao 2-1 ndipo wakaibadili jina la Utete na kuipa jina la Liverpool kwa kuwa walikuwa ni wanachama wa Liverpool wakaikabidhi Utete na ile zawadi ya ngao…
“Wakati ule Utete inashiriki ligi ya wilaya ambayo ndio ilikuwa Ligi ya Mkoa, ilishirikisha timu za Sunderland, Cosmo, Yanga na timu nyingine na wakaibadilisha wakaiita Liverpool na hapo ndio ikacheza Ligi Kuu kwa jina la Liverpool mwaka 1970,” anasema China.
“Serikali kupitia kwa Rais Abeid Amani Karume miaka hiyo ya 70 akasema timu zote zenye majina ya kigeni zibadilishwe ziitwe majina ya kwetu tuachane na majina ya kizungu sisi ndio tukaamua kujiita Ashanti Football Club, Sunderland ndio ikabadili na kuitwa Simba... “Mwaka 1993, Ashanti iligawanyika ilitokea mpasuko mkubwa kati ya wachezaji wakongwe na wanachama hivyo kukawa na Ashanti na Utete ‘Msimbazi Rovers au ‘Pentagon’,”.
“ Kulikuwa na michuano ya ‘Maharage’ maarufu Ndondo ilifanyika Msimbazi Center ilishirikisha timu ya Gereji wakati Utete katika mashindano yale walitumia jina la Msimbazi Rovers a.k.a ‘Pentagon’… “Sasa michuano ile wachezaji waligawanyika wapo walioenda kuchezea timu ya Gereji ambayo maskani yake ilikuwa sokoni Ilala, na wengine wakabaki Msimbazi Rovers ambayo maskani yake yalikuwa Ilala mtaa wa Utete Katika mashindano hayo Gereji walifungwa mabao 2-1 sasa mashindano yalipoisha bado kukawa na bifu kubwa, mpaka kwa familia timu ikasambaratika.
“Mashabiki nao waligawanyika mtaa wa Utete na Morogoro wakaunga mkono Gereji na baadhi ya watu wa Utete na mtaa wa Arusha wakaiunga mkono Pentagon… “Pentagon ndio walijitoa wakasema wanaanzisha timu yao hawataki tena kurudi Ashanti, wakawa wanafanya mazoezi kwenye uwanja wa Karume, viongozi wa Ashanti wakaenda kuwavua bukta, kuwapokonya vifaa vya timu, wakati huo viongozi walikuwa marehemu Mwijuma Mkange (Mwenyekiti) na Juma Moto (Katibu)...
“Benchi la ufundi la Ashanti nalo likasambaratika, kocha alikuwa Mbaraka Hassan akaenda kuifudisha Pentagon, wakacheza kuanzia ngazi ya Wilaya, mkoa na kufanikiwa kupanda Ligi Kuu, wachezaji wakati huo ni wakina Almas Kasongo (Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam), wakacheza msimu wa kwanza Pentagon ikashuka daraja, tena walipanda na JKT Ruvu ambayo mpaka leo haijashuka daraja, na Gereji nayo huku ikiwa ni kama imekufa.
“Baada ya hapo tuliamua kukaa chini na kuzungumza tukaweka tofauti zetu pembeni na kuunga tena Ashanti United na tukafanikiwa kuipandisha Ligi Kuu mwaka 2004, msimu wa pili wa mwaka 2007 ndio tukashuka daraja. “Baadae tukapanda, tukashuka mpaka Wilayani, mwisho kukawa hakuna mtu anamuda na timu lakini baadae tukaamua tena kukaa chini na kuipandisha timu yetu daraja”.
Kusota ligi daraja la kwanza “Ligi mwaka jana daraja la kwanza tulimaliza wa pili tulitakiwa tumfunge African Lyon, wao walikuwa wanasaka sare, bahati mbaya wakatufunga wakapanda, kilichotufanya tukashindwa ni ukata, wachezaji walihitaji fedha, mpira wa Tanzania umejaa rushwa, mazingaombwe,” Anadai China.
“TFF ni taasisi wala haimiliki wachezaji inategemea kutoka kwa klabu, ukiingia Ligi Kuu lazima uwe na timu ya vijana nitapata wapi fedha za kuwalipa mishahara wao tulionao tu hatuna fedha za kuwapa bado tukaongeze wengine... “Ligi Tanzania mzunguko wa kwanza ukipoteza mechi tano ujue umekwenda na maji, mzunguko wa pili ni mauzauza kwa sababu zipo zinazotaka kupata ubingwa na nyingine kujinusuru kushuka daraja,” anasema.
Ukata
Akizungumzia kuhusu hilo, China anasema: “Simba na Yanga zinakosa wadhamini sisi watu wa chini tutapata wapi, watu wanaingia kwa ubabaishaji wao tungekuwa na wadhamini wa kueleweka hata Ligi yetu ingekuwa mbali. Anasema mpira unahitaji fedha, Ashanti inamashabiki wengi ukiondoa Simba na Yanga inayofuatwa ni Ashanti, lakini ukata ndio unaowamaliza. Gharama Anasema mazoezi gharama sh 120,000 kila siku.
Wachezaji
Wachezaji posho Sh 3,000 makocha Sh 5,000 fedha ni nyingi watazipata wapi pasi na udhamini. “Mishahara hatulipi, hakuna mchezaji anayechukua mshahara na wala hatuna bajeti hiyo, na sio Ashanti tu hata Friends Rangers hizi timu zinaishi hivyo, kama mtu anamatatizo tunamsaidia kwa kuchangishana lakini sio mshahara hakuna uendeshaji mkubwa sana,” anasema.
Wauza Mitumba/Michango mashabiki
“Tunawachangisha kwenye kitabu kila siku waichangie tu ndio tunapata hiyo Sh 120,000 ya kuwalipa posho, na michango inaanza Sh 500 kuendelea kila mtu anatoa kulingana na uwezo wake, hata hivyo kuna siku unapata yote kuna siku hupati. “Hata hivyo Ilala imegawanyika kuna timu nyingine ya Bomu ipo mtaa wa Arusha sasa hata kwa mashabiki wamegawanyika wengine wa Bomu wengine wa Ashanti Mungu akijalia timu zote mbili zikipanda daraja, kuna upinzani mkali sana utakuwepo ukiacha wa Simba na Yanga,” anasisitiza China.
Kwa upande wa Kocha wa Ashanti Mbaraka anasema: “ Ukata ni sehemu ya maisha yetu, sisi tumeshazoea ingawa shida haizoeleki, ila sisi imebidi tuzoee, yoyote atakayeitembelea timu yetu ni lazima achangie hata jero (Sh. 500), gurudumu liende,”
Waliteleza “Ligi daraja la kwanza ni ngumu, mfano kundi letu lilikua na timu saba msimu uliopita, inayotakiwa kupanda ni moja, tunajitahidi lakini ndio hivyo tunakwama, tulipanda daraja kwa mara ya kwanza mwaka 2004 ikiundwa na wachezaji kama Juma Nyoso, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ Abdulharim Humoud, na wengine makosa, unapoteleza wenzako wanatumia makosa yako na kusonga mbele ndicho kilichotukuta na kufanya tuendelee kusota,” anasema.
Ashanti Mwaka 2010/2011 ilishuka daraja na kukaa msimu mmoja kabla ya kupanda tena Ligi Kuu na kushindwa kufurukuta ikajikuta inashuka tena daraja msimu wa mwaka 2013. “Tunajipanga kuhakikisha msimu huu unaoanza tunapanda daraja, tunaweka mipango imara timu yetu si timu ya wahuni, wala wafanya fujo, sisi ni watu wa malengo, ila ukata ndio unaotusumbua kwa sana, lakini viongozi wanapigana kuendesha timu.

No comments: