Advertisements

Monday, April 24, 2017

MCHUNGAJI MBARONI KWA KUFICHA WAHAMIAJI

Mahakama ya Arusha.
MCHUNGAJI wa Kanisa la Ukombozi Pentecoste lililopo eneo la Sakina jijini hapa, amekamatwa na maofisa wa Uhamiaji baada ya kubainika kuwaficha wahamiaji haramu kutoka Lubumbashi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mchungaji Danson Kabwebwe (37), amekamatwa pamoja na wenzake wawili, mmoja akiwa ni mwanamke, Anna Buibui Kambey ambaye pia alikuwa anajulikana kama Anna John Mollel (47), pamoja na mtu mwingine, Harrison John Laizer (30).

Wote kwa pamoja wanadaiwa kuwaingiza na kuwaficha nchini raia watatu wa DRC ambao ni Glory Mwanza Lubingo na mkewe Linda Mbaki Diangwe pamoja na binti yao, Berenice Glory. Wakongo hao waliingia nchini tangu Novemba 2015 na wakaendelea kuishi jijini Arusha kinyume cha sheria kwa miaka yote mitatu.

“Lakini siyo hivyo tu, huyu Mchungaji wa Kanisa la Ukombozi Pentecoste, alikuwa mbioni kuwatengenezea wahamiaji hao pasi za kusafiria za Tanzania na tuliwagundua wakati wakiwa kwenye utaratibu wa kufuatilia pasipoti hizo,” alisema Ofisa Uhamiaji mkoani Arusha, Ally Dadi.

Ni katika sakata hilo ndipo ikagundulika pia kuwa, mchungaji wa Kanisa hilo la Ukombozi alikuwa akitumia ofisi yake kutengeneza vyeti feki vya kuzaliwa, na tayari alikuwa amewaandalia Wakongo hao makaratasi muhimu, vikiwemo vyeti feki vya kuzaliwa na vya ubatizo, pamoja na barua za watendaji kata.

Kama wangefanikiwa basi Glory Mwanza Lubingo kutoka Congo angegeuka kuwa ‘Glory Harrison Kimaro,’ huku mkewe, Linda Mbaki Diangwe angefahamika kama ‘Linda John Khuley,’ wakati mtoto wao alikuwa apewe jina la ‘Berenice Glory Kimaro!’ Tayari vyeti feki vya ubatizo vyenye nembo ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Moshi vilikuwa vimeandaliwa, pengine kuonesha kuwa watuhumiwa hao watatu kutoka Lubumbashi nchini DRC walikuwa ni wazaliwa wa Mkoa wa Kilimanjaro.

“Tayari tumekamilisha upelelezi na wahamiaji hawa haramu, pamoja na Watanzania waliokuwa wakiwaficha hapa Arusha watapelekwa mahakamani,” aliongeza Dadi. Alielezea kusikitishwa kwake na kitendo cha viongozi wa dini, watu wanaoaminika na kuheshimika na jamii, kujihusisha na uhalifu ambao ungeweza kabisa kuhatarisha usalama wa nchi na watu wake.

HABARI LEO

No comments: