Advertisements

Monday, April 24, 2017

MGOGORO CUF WAZIDI KUWAKA MOTO

By Waandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mgawanyiko ndani ya CUF umeendelea kutikisa baada ya Jeshi la Polisikuzuia mkutano wa ndani uliotakiwa kufanyika jana kutokana na vurugu zilizotokea juzi, huku upande wa Profesa Ibrahim Lipumba ukikanusha kuhusika katika shambulio hilo.

Upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad unautuhumu upande wa Profesa Lipumba kuhusika na shambulio hilo.

Wabunge wanane wa CUF, Jukwaa la Wahariri (TEF) na Baraza la Habari (MCT) wamelaani shambulio hilo, wakitaka hatua zichukuliwe, huku Jeshi la Polisi likisema halijamkamata mtu yeyote kuhusika na kitendo hicho, zaidi ya mtu aliyedhibitiwa na wananchi.

Juzi, watu waliotumia gari lililokuwa na nembo ya CUF, walivamia mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na viongozi wa chama hicho wilayani Kinondoni, na kuwapiga huku mmoja wa wavamizi aliyejifunika uso kwa kofia mithili ya soksi, akichomoa bastola kutishia.

Mmoja wa wavamizi hao alishindwa kuondoka na wenzake Hoteli ya Vina iliyoko Mabibo na hivyo kupigwa na wananchi waliokuwa wakijongea eneo hilo baada ya kusikia kelele za kuomba msaada.

Mkutano wa mbunge wazuiwa Dar

Kutokana na vurugu hizo Jeshi la Polisi limezuia mkutano wa Mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea uliokuwa ufanyike jana kwa madai kuwa wanachama wa CUF upande wa Profesa Lipumba wameweka pingamizi.

“Jana (juzi) saa 8:00 mchana nilipata barua ya zuio la kikao hiki kutoka polisi. Wamenieleza kikao hiki kimepingwa na wanachama hao wa Profesa Lipumba na kwa sababu za kiusalama. Ni bora kisifanyike,” alisema Mtolea.

Mtolea alisema aliitisha kikao hicho kama mbunge wa jimbo hilo na aliwashirikisha baadhi ya wajumbe wa CUF na kumualika Maalim Seif.

Alisema baada ya kikao hicho kuzuiwa, wanajiandaa kwenda Buguruni Jumapili ijayo kufanya shughuli zao za kichama kwa kuwa hiyo ni haki yao.

Kuhusu kuzuiwa kwa kikao hicho, kamanda wa polisi wa Temeke, Gilles Muroto alisema wamechukua uamuzi huo kwa sababu za usalama pia kwa faida ya mbunge na chama chake.

Kuhusu waliohusika katika shambulio la juzi, naibu katibu mkuu wa chama hicho, Nassor Mazrui alisema kitendo cha wafuasi wa Profesa Lipumba kuvamia na kufanya vurugu kwenye mkutano huo ni aibu kwa Tanzania katika medani za kimataifa.

Alisema hajui wafuasi wa Profesa Lipumba wanajiamini nini hadi kuvamia mkutano huo na kuwapiga wanachama na waandishi wa habari wakati vyombo vya dola vipo.

“Wafuasi wa Profesa Lipumba sasa wanafanya uhalifu mchana kweupe bila ya hofu, wanalindwa na nani?” alihoji Mazrui.

Mazrui alisema Jeshi la Polisi ni lazima liwasake wahalifu hao na kuwachukulia hatua ili kuliepusha taifa na aibu ya aina hiyo.

“CUF tunafanya siasa za kistaarabu lakini kikundi cha watu wachache wanatuletea vurugu ili tuonekane hatufai. Vitendo kama hivyo ni aibu kwa Tanzania nzima,” alisema.

Akizungumzia vurugu hizo, mwenyekiti wa kamati ya uongozi wa CUF, Julius Mtatiro alilaani na kuwataka waandishi waliokuwepo kwenye tukio hilo kumkabidhi picha za video na mnato ili zisaidie kuwasaka wahusika.

“Ni lazima tuwasake wahusika na kuweka picha zao hadharani. Uovu huu hauwezi kudumu na kamwe hatuwezi kuukalia kimya,” alisema.

Timu ya ya Lipumba yakana

Hata hivyo, mkurugenzi wa habari na mawasiliano kwa umma wa CUF upande wa Lipumba, Abdul Kambaya alisema hawahusiki na uvamizi huo.

Alisema uongozi wa chama hicho unakutana na utazungumzia suala hilo kwa ajili ya kuupatia umma taarifa.

“Mimi nilidhani utaulizia walioumizwa kwa kukatwa visigino, wewe unataka kujua kwamba tunahusika vipi katika vurugu?’’ alisema.

Hata hivyo, alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa watu hao walioumizwa kama ni wafuasi wao, alisema aachwe kwanza kwa sababu chama kipo kwenye kikao na kukata simu.

Jeshi la Polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Kinondoni, Suzan Kaganda alisema hakuna anayeshikiliwa na polisi kwa kuhusika na tukio hilo.

“Aliyebainika ni yule jamaa aliyepelekwa Hospitali ya Muhimbili ambaye alipigwa na wananchi pale eneo la tukio Mabibo, lakini wengine hawajakamatwa bado,” alisema Kaganda.

Alisema polisi itatoa taarifa iwapo watu watakamatwa kuhusika na vurugu hizo.

Kuhusu mtu aliyeshika bastola na kuwatishia watu waliokuwa kwenye mkutano huo na kusababisha wengine kuumia wakiwamo waandishi wa habari, Kaganda alisema hana taarifa.

Jukwaa la wahariri


Shambulio hilo limelaaniwa na taasisi tofauti.

Makamu mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alisema kitendo cha wanasiasa kuwatumia waandishi kama ngazi lakini hawawapi ulinzi, kinasikitisha.

Alisema waandishi walitakiwa kupewa ulinzi kwa sababu kazi yao ni kuhabarisha jamii, lakini inapotokea wanashambuliwa ni ukiukwaji wa utaratibu wa vyama vya siasa.

Baraza la Habari

Lakini katibu mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga alisema tatizo kubwa la wanasiasa ni kuwaingiza waandishi katika tofauti zao na kuwasababishia matatizo.

Alisema pia vyombo vya usalama vinatakiwa kuelimishwa kuwa waandishi wana haki ya kulindwa wanapokuwa katika kazi zao na si kuwaacha washambuliwe.

Aliwashauri wahariri kuhakikisha wanawatuma waandishi wawili kwenye mikutano ya aina hiyo kwa ajili ya kuimarisha usalama badala ya kumtuma mmoja.

Msajili wa Vyama

Alipotafutwa ili kuzungumzia vurugu hizo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi hakupatikana. Hata hivyo, Naibu Msajili, Sisty Nyahoza aliomba apewe muda ili awasiliane na bosi wake, lakini baadaye hakupatikana.

Imeandikwa na Regnald Miruko, Raymond Kaminyoge, Hussein Issa na Bakari Kiango

No comments: